Kiungo wa Dinamo Bucharest na Cameroon Patrick Ekeng amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 25 kwa kile kinachodhaniwa ni shambulio la moyo baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mechi.
Ekeng alianguka chini dakika ya 70 wakati wa mchezo wa ligi ya Romania kati ya Dinamo Bucharest dhidi ya Viitorul.
Saa mbili baadaye zilitoka habari kutoka hospitali kwamba Ekeng amefariki. Shirikisho la Soka la Romania limetangaza kusogeza mbele kwa wiki moja zaidi mchezo wa fainali ya kombe la FA (Romanian Cup) kati ya Dinamo na Cluj na sasa utachezwa May 17.
Ekeng alijiunga na Dinamo Bucharest mwezi January akitokea katika klabu ya Cordoba ya nchini Hispania.
Imetangazwa kuahirishwa kwa mechi zote ambazo zilikuwa zichezwe weekend hii. Chama cha soka cha Cameroon kimethibitisha kifo cha Ekeng kupitia mtandao wa twitter huku klabu yake ya zamani ya Cordoba ikitweet pia kusikitishwa na taarifa za kiungo wao huyo wa zamani: “hatuna maneno ya kuelezea huzuni tuliyonayo kutokana na kifo cha Ekeng”.
Ekeng amewahi pia kucheza kwenye vilabu vya Le Mans na Lausanne. Mwaka 2003, kiungo wa kimataifa wa Cameroon Marc-Vivien Foe alifariki baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mchezo dhidi ya Colombia kwenye michuano ya Confederations iliyofanyika Ufaransa.
No comments:
Post a Comment