Zaidi ya wafanyabiashara wadogo 2,000 waliokuwa wakifanya shughuli zao maeneo yasiyo rasmi katika Manispaa ya Ilala, wametengewa masoko manne kwa ajili ya kufanya biashara.
Masoko hayo ni Kigogo Fresh lililopo eneo la Pugu, Ukonga karibu na gereza, Tabata Muslim na Kivule ambayo wafanyabiashara hao maarufu kama wamachinga wanatakiwa kwenda.
Wafanyabiashara waliolengwa zaidi ni wale ambao wanafanya shughuli zao kwa kupanga barabarani, hususan barabara ya mabasi yaendayo haraka na katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo na Mnazi Mmoja kwenye manispaa hiyo.
Baadhi ya wafanyabishara hao walionyesha wasiwasi wao juu ya uamuzi huo kuwa masoko hayo siyo rafiki kwao kwa biashara wanazozifanya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgurumi alisema jana kuwa, utaratibu wa kuwapangia maeneo wafanyabiashara hao ulichelewa kwa sababu walikuwa katika mchakato wa kuwatambua ili mpango wa kuwapeleka ufanyike kwa ufanisi.
Alisema mazingira ya masoko hayo manne yapo vizuri na yana uwezo wa kumudu wafanyabiashara zaidi ya 2,000 na makadirio ni wafanyabiashara 6,000.
Kwa mujibu wa Mngulumi, kesho, manispaa ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama itaanza operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu.
“Hapa ni kama nakazia tu uamuzi huu, ila tulishawatangazia awali. Kwa hiyo sitarajii kuona watu maeneo hayo kesho, operesheni hii itaenda sambamba na kuwaondoa wenye gereji bubu na wanaoosha magari,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment