Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewasimamisha kazi wakuu wawili wa idara katika manispaa mbili kwa tuhuma za kushindwa kutoa maelezo kuhusu watumishi hewa katika idara zao, huku wakiendelea kuidhinisha mishahara yao kwa miaka mingi.
Makonda aliwataja watumishi hao waliosimamishwa kazi kuwa ni Mkuu wa Idara ya Utumishi wa Manispaa ya Ilala, Francis Kilawe na Mkuu wa Idara ya Afya Temeke, Syrivia Mamkwe na kuagiza uchunguzi dhidi ya tuhuma zao ufanyike haraka.
Kiongozi huyo alichukua uamuzi huo baada ya hivi karibuni kuwaapisha wakuu wa idara kutoka manispaa tatu ili kusema ukweli na kuwapa wiki moja kuhakiki watumishi hewa katika maeneo yao ya kazi.
Makonda alisema hadi kufikia jana, jumla ya watumishi hewa 39 waligundulika na kufikisha 248 kutoka 209 wa takwimu za awali.
Kati yao, 26 wanatoka Ilala, wawili (Kinondoni) na 11 (Temeke) na kulisababishia jiji hilo kupata hasara ya zaidi Sh3 bilioni.
“Kilawe ameshindwa kujieleza kuhusu watumishi hewa 11 ambao hajui wako wapi, lakini wanapokea mishahara tangu mwaka 2010.Huku yeye akisaini mishahara yao,” alisema Makonda.
Makonda ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni aliongeza kuwa Mamkwe alishindwa kujieleza walipo watumishi hewa wawili ambao bado wanaendelea kupata mishahara huku akiwa kiongozi wa idara husika.
Kutokana na hali hiyo, Makonda amewaongezea wiki mbili maofisa wanaochunguza suala hilo ili kuwabaini zaidi watumishi hewa kwa madai kuwa bado wanaonekana katika mfumo wa kupokea malipo kutoka Hazina kwenda katika manispaa.
“Huu ndiyo mkutano wangu wa mwisho kwenu.Wiki hizi mbili zikiisha tutaanza uchunguzi dhidi yenu na tukibaini watumishi hewa katika idara yako utawajibishwa ,” alisema Makonda ambaye pia ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM.
No comments:
Post a Comment