Moshi mweusi uliokuwa unafuka katika jalala lililokuwa linachomwa ulifanya mfano wa ukungu usiopendeza machoni.
Wapita njia waliongeza mwendokasi walivyokaribia eneo lile. Wengine waliziba pua zao kwa kutumia viganja vya mikono yao kuepukana na hewa hiyo chafu.
Baadhi yao walijiziba kwa kutumia vipande magazeti, wengine kwa bahasha zao. Ilikuwa ni jioni na kila mmoja alikuwa anarejea kutoka katika mizunguko yake ama popote pale ajuapo mwenyewe na nafsi yake. Ilimradi hekaheka na kila mmoja kutingwa na lake!!
Kwa jinsi watu walivyokuwa wametingwa na mambo vichwani mwao hawakuweza kulishuhudia kundi la viumbe hai ambalo halikubabaishwa na moshi huo mzito ambao ulionekana kuzua karaha kwa wapiti njia wengine. Na hata kama wangeona wasingekuwa na la kusaidia zaidi ya kupata la kuongea na kujisahaulisha suluba ya siku nzima huko walipotoka. Nani wa kumjali mtoto wa mwenzake katika mji huu!!
Ardhi iliyobeba uchafu wa kila aina iliyopewa jina la jalala ilikuwa katika mahangahiko ikifukuliwa kwa fujo na watoto wanne wa rika moja huku mkubwa akikadiriwa kuwa na miaka kumi na mitano
Macho yao yalikuwa mekundu, matambala ambayo zamani yaliitwa nguo yalifunika miili yao ilimradi tu kujistiri!!
Wengine walikuwa wameinama wengine wakiwa wamepiga magoti, mikono yao ikiwa imejikita katika kuchimba ardhi na kutoka na vyuma chakavu.
Matambala waliyovaa yaliwafanya wote wafanane, na ilikuwa ngumu kutambua iwapo wana jinsia tofauti.
Hakuna aliyezungumza na mwenzake, nyuso zao zilizotiririka jasho zilitangaza njaa kali na chuki. Na kila mmoja alikuwa katika kuutafuta mkate wake wa siku hiyo, mkate uliopatikana kwa kuuza vyuma vile chakavu.
Mtoto mmoja kati ya hao wane alivyojiridhisha kuwa eneo lile vyuma vilikuwa vimekwisha ama vilikuwa vimejikitasehemu ngumu kufikika, alinyanyuka na mfuko wake wa chumvichumvi, akachukua mkono wake mchafu akajipangusa jasho. Tambala alilokuwa amevaa lilisomeka kwa shida maandishi 'I LOVE TANZANIA', lilikuwa kubwa kumpita na lilikuwa limetatuka na kuruhusu maziwa yake yaliyokuwa yameanza kujifunza kusimama yachungulie nje. Huyu pekee alikuwa mkubwa kupita wenzake. Na ni hapa ungeweza kutambua kuwa alikuwa msichana.
Alijikongoja na fuko lake hadi akalifikia jalala jingine. Hapo pia alipapasa bila kupata chochote. Akasimama wima akiwa amekata tamaa. nuru ilizidi kutowekana kama hali ingeendelea hivyo basi angejihakikishia kulala njaa. Alipopiga hatua nne kuliacha jalala macho yake yalivutiwa na kifurushi cha uchafu wa siku nyingi, akatua tena fuko lake akachukua kimti kigumu akaliendea lile furushi katika namna ileile ya kukatatamaa kisha kuanza kupekenyua.
Lahaula!
Tabasamu pana likachanua usöni mwake, akayapongeza macho yake kwa kuvutiwa na furushi lile huku akiushukuru mwili wake pia kwa uvumilivu. Akavuta kwa nguvu, akatoka na jembe chakavu lililokuwa limejizika katika uchafu ule kwa siku nyingi.
Biashara nzuri kwa siku hiyo! Na uhakika wa kupata chakula cha siku hiyo ulikuwepo. Kilichofuata baada ya bahati hiyo ya mtende ni kutafuta mahali sahihi ambapo anaweza kuuza chuma kile chakavu apate shilingi kadhaa kwa ajili ya chakula.
Wakati anasimama kuliendea fuko lake, akasita kabla ya kupiga hatua. Hakuwa peke yake eneo lile, kuna mtu alikuwa akimfuatilia kwa ukaribu kabisa.
"Siso yangu hiyo!" sauti ya kiume ilikoroma. Binti akamtazama yule chokoraa mwenye nywele zinazotaka kufanana na mwarabu, ngozi nyeusi yenye ukurutu unaotiririka jasho.
"Siso yangu hiyo uliyoshika" sauti ya mvulana haikuwa na mzaha. Alimaanisha!
Yule binti akashtuka na kulitazama lile jembe chakavu mkononi kana kwamba hakutambua kama amelishikilia, kisha akapuuzia akapiga hatua kadhaa kuliendea fuko lake, yule kijana akamfanyia shambulizi la kushtukiza, akamnyakua lile jembe. Alipotaka kukimbia yule binti akawa mwepesi akakamata shati chakavu la yule kijana. Kama vile wembe mkali unavyokutana na karatasi laini ndivyo lilivyoachana tambala lile.
"Mamaa! Umenichania shati we malaya!"
"Nani malaya? Malaya mama yako aliyekuzaa akakutupa jalalani mwanahizaya mkubwa nipatie jembe langu!" binti naye alijibu mapigo kwa sauti kali. Tusi hilo likamgusa yule mpinzani wake.
Pasipokutegemea alivamiwa na kuchabangwa teke tumboni kwa nguvu, akajipindua na kuanza kuugulia maumivu. Tambala lililokuwa linamuhifadhi likakosa umakini, nguo yake ya ndani ambayo zamani ilikuwa nyeupe lakini sasa ikiwa kama ina kutu ilichungulia nje. Mbavu zake zilizohesabika kutokana na wembamba na udhaifu wake kiafya zilitokeza nje.
Yule mhanga wa kuchaniwa shati kisha kutukanwa akiwa hajaridhika na pigo lile alimrukia tena akamchabanga teke kali katika zile mbavu zilizokuwa nje kimakosa, sasa binti akanyoosha mikono kuomba msamaha huku maumivu yakiukunja uso wake. Alikuwa kama anayelia kwa sauti ya juu lakini sauti ikigoma kutoka.
Hakuupata msamaha bali kukaribisha kipigo kingine. Tumboni tena! Nani wa kumsaidia wakati lilikuwa tukio la kawaida wao kwa wao kurumbana na kisha kupigana.
"Mariaa! Mariaa!" sauti kali ilisikika kutokea katika ule moshi mzito upande wa pili.
Maria aliyekuwa amekumbatia uchafu wa jalalani alisikia lakini hakuweza kugeuka. Mbavu zilikuwa zinamuuma na alipumua kwa shida sana. Alitamani kulia kwa sauti kuu, lakini sauti ikagoma kutoka.
Vishindo vya miguu vikafika karibu yake. Akaishia kuiona miguu lakini hakuweza kumuona mwenye hiyo miguu.
"Kwanini unampiga?
"Kwanini unampiga?" sauti ya kitoto ililalamika kwa uchungu. Ni sauti hii ya mtu aliyesimama pembeni yake.
"Kwani na wewe dogo unasemaje?" alijibu kwa ubabe na jeuri yule mhanga wa kuchaniwa shati.
Maria alisikia kila kitu lakini hakuweza kuongea. Alitamani yule mtoto angekuwa mtu mzima huenda angemsaidia.
Yule kijana ambaye alikuwa kama amepandwa na mori ya kimasai, alijitazama tena shati lake lililoachana, hasira ikapanda upya!
Akampuuzia yule mtoto. Akamrukia Maria. Sasa aliamua kutumia mikono.
"Utalipa shati langu utalipa we malaya." maneno hayo hayakutoka bure, yalisindikizwa na mdundo wa mapigo ya ngumi na vibao katika uso wa Maria, ambaye naye tambala lake lilikuwa limeuacha mwili. Kifua chake kikatazamana na mbingu za bluu.
Hapa likatokea tukio lisilotarajiwa na wote mpiga na mpigwa.
Yule mtoto mwenye umri wa miaka tisa aliyekulia katika kundi maarufu na hatari jijini Mwanza la 'watoto wa wakoma' alichomoka mbiombio akamfikia mpigaji.
Kitendo cha sekunde tatu hali ikabadilika. Maria akabaki huru, yule mpigaji akatua chini akiwa anagalagala, damu ikiruka kwa fujo mgongoni mwake. Mtoto wa wakoma alikuwa anatoweka kuelekea mashariki.
Wembe wenye makali ulikuwa umepenya katikati ya mgongo wa yule mpigaji.
****
MKASA UMEANZIA HAPA……
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment