Mbwana Samatta amecheza dakika zote 90 za mchezo kati yake ya Genk dhidi ya Anderlecht na kuisaidia Genk kuibuka na ushindi wa magoli 5-2 katika kampeni za kuhakikisha timu yao inapata nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League.
Anderlecht walianza kufunga goli la kuongoza dakika ya 25 kupitia kwa kiungo wao Filip Djuricic lakini goli hilo lilisawazishwa na Leon Bailey dakika ya 45 na kuufanya mchezo huo kwenda mapumziko timu zote zikiwa sare kwa kufungana goli 1-1.
Kipindi cha pili Suarez aliiweka tena mbele Anderlecht kwa kuifungia bao la pili dakika ya 60 lakini dakika tano baadaye Buffel aliisawazishia Genk. Dakika ya 76, Pozuelo aliiweka mbele Genk kwa kutupia bao la tatu kisha Ndidi akaongeza bao la nne kabla ya Nikos Karelis hajamaliza shughuli kwa kufunga goli dakika ya 90 ya mchezo.
Samatta kucheza dakika zote 90 ni faraja kubwa kwasababu mchezo uliopita alitolewa kipindi cha kwanza wakati Genk ilipocheza na KV Oostende.
Samatta amesema sababu kubwa iliyopelekea kushindwa kuendelea na mchezo ule ilikuwa ni majereha aliyoyapata wakati wa kipindi cha kwanza cha mechi hiyo.
“Mechi iliyopit nilipata majeruhi kwenye kipindi cha kwanza cha mechi hiyo, niliumia eneo la nyonga kwa hiyo baada ya kurudi vyumbani na kuwaeleza madaktari, waliniambia nipumzike kwasababu ningeweza kuendelea lakini wasiwasi ukawa ni kwamba huenda majeraha yangeongezeka halafu ingechukua muda zaidi kupona”.
“Kwahiyo madaktari waliamua nipumzike baada ya kupata maumivu, madaktari walijitahidi nipone haraka kwa ajili ya mchezo wa leo na jana nilifanya mazoezi pamoja na timu, kucheza au kutocheza kwenye mchezo wa leo ilikuwa ni mipango ya mwalimu.”
Endapo Genk watashinda mchezo wao wa mwisho siku ya Jumapili, watafuzu moja kwa moja kucheza Europa League lakini kama watamaliza wakiwa nafasi ya nne basi watalazimika kucheza play off nyingine dhidi ya mshindi wa play off II kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Europa.
No comments:
Post a Comment